
| Shule ya sekondari Pwani inayomilikiwa na jumuiya ya wazazi ya chama cha mapinduzi (CCM) Mji wa Kibaha ,inayodaiwa kuuzwa kwa SUA Morogoro,huku viongozi wa jumuiya wilaya wakiwa hawajashirikishwa ambapo shule hiyo ,kwasasa imegeuka malisho ya ng'ombe.(Picha na Mwamvua Mwinyi) |
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
SHULE ya sekondari ya Pwani,inayomilikiwa na jumuiya ya wazazi ya chama cha mapinduzi(CCM)Mji wa Kibaha ,iliyopo kata ya Tangini,inadaiwa kuuzwa pasipo kushirikishwa viongozi wa kata na wilaya.
Shule hiyo inadaiwa kuuzwa pamoja na shamba la jumuiya hiyo lililopo Simbani ,vinasadikiwa kuuzwa kwa SUA Morogoro kwa gharama ya mil.300 .
Mali hizo zimeuzwa kipindi kifupi baada ya uongozi wa CCM taifa kuagiza mali za jumuiya na chama ngazi zote kuhakikiwa na kuhakikisha zinalindwa .
Wakizungumza leo,kwa nyakati tofauti ,baadhi ya wanachama wa jumuiya ya wazazi wilayani humo,walisema mbali ya hayo, kuanzia jumuiya ngazi ya tawi,kata,wilaya na mkoa inaelezwa havijapata asilimia yoyote ya fedha hizo .
Walisema mali hizo zimeuzwa kiutata kutokana na hata viongozi wa jumuiya na chama wilaya wapo kwenye sintofahamu.
Alieleza kuwa ,katika zoezi la uhakiki wa mali za chama ndio ilipogundulika kuuzwa kwa vitu hivyo na kusababisha malalamiko ya vikao kutojua suala hilo na kukosa taarifa kamili .
Andrew Lugano alisema ,shule hiyo ilikuwa ni msaada mkubwa kwa watoto wao wenye wazazi wa kipato cha chini.
Alisema shule hiyo imefungwa hivyo wanafunzi waliokuwa wakisoma shuleni hapo wahamishwa na wazazi wao maeneo mengine ambapo wanapata usumbufu mkubwa kwani eneo hilo halina shule ya sekondari ya jirani.
Lugano alisema ni miaka mitano sasa shule hiyo ni kama ilifungwa na kwasasa imeuzwa pasipo kufuata utaratibu wa ushirikishwaji.
"Wakati nikiwa diwani wa kata ya Mailmoja ,shule hii awali ilitaka kukodishwa kwa kiasi cha sh.mil.12 kwa mwaka lakini tulizuia ,lakini kwasasa naona azma iliyotakiwa ndio imefanikiwa" alisema Lugano.
Wanachama wengine wa jumuiya hiyo tawi la Tangini ,walisema walipata taarifa kuna barua imetoka ngazi ya Taifa, kuwa shule hiyo kwasasa imeuzwa kwa chuo cha kilimo SUA .
"Badala ya kufuata vikao ama viongozi wetu kushirikishwa baada ya barua yenye maagizo kutoka juu Taifa ,viongozi ngazi ya wilaya walitakiwa kushiriki kuonyesha mipaka ya shule hiyo pekee".
Nae katibu wa wazazi kata ya Tangini ,Ramadhani Mkekema ,alisema hajashirikishwa mchakato huo wa mauziano zaidi ya kuombwa akashiriki katika kuonyesha mipaka na makabidhiano.
Alisema siku ya tukio alipigiwa simu na katibu wa wazazi ,Mji wa Kibaha ,Ruth Mtashaba ,kuwa akaonyeshe mipaka halisi ya eneo la shule na baada ya hapo alishuhudia kuuzwa kwa eneo.
Mkekema alieleza kuwa aliambiwa eneo sio lao kuanzia sasa,ambapo alidai hela zake alipwe za kufanya usafi na kulinda eneo hilo la shule.
" Mimi nilikuwa nalinda na kusafisha eneo hili ndipo nilipoona limeuzwa nikaona niseme deni langu kabina na kujua nitalipwa na nani"
"Nilielezwa nitalipwa na SUA kuanzia siku hiyo na chakushangaza hadi leo japo niliwapa namba zangu hawajanilipa hela za nyuma wala sasa" alisema Mkekema.
Kwa upande wake katibu wa wazazi mji wa Kibaha ,Ruth Mtashaba alipotafutwa agost 23 kutoa ufafanuzi na mwenyekiti wake Athumani Mokiwa ofisini kwao hawakuwepo .
Juhudi za kuwatafuta kwa njia ya simu Mokiwa ,alisema hawezi kuliongelea suala hilo bali atafutwe katibu wake .
Ruth alipoulizwa alisema hawezi kuongea lolote na atakaejibu suala hilo ni katibu wa Jumuiya ngazi ya mkoa na pia yeye anaumwa .
Kaimu katibu wa Jumuiya hiyo ngazi ya mkoa wa Pwani aliyejulikana kwa jina la Hassan Sharifu alipopigiwa simu kuulizwa , taarifa hizo alisema taarifa zote zipo ngazi ya Taifa na kwa chochote anayeweza kuongelea ni katibu ngazi ya Taifa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mji wa Kibaha,Maulid Bundala alisema ni kweli wamepokea taarifa kutoka jumuiya ya wazazi wilaya kuwa shule hiyo imeuzwa.
Alisema wamesikitika kuuzwa kwa shule hiyo kwani hakukuwa na haraka ya kufanya hivyo kutokana na thamani ya ardhi kupanda kila siku.
Bundala alisema walitaarifiwa na katibu huyo kuwa uongozi wa juu wa jumuiya ya wazazi taifa yaani katibu mkuu wa jumuiya hiyo aliwaandikia barua shule hiyo imeuzwa na ikabidhiwe kwa aliyeuziwa ambapoi yeye kama mwenyekiti wa CCM hamjui aliyeuziwa.
Alisema ,kama uongozi wa wilaya waliomba nakala ya taarifa ya barua hiyo na kamati ya siasa wilaya inajua lakini mnunuzi na gharama wanajua jumuiya hiyo.
Bundala alisema barua hiyo imeonyesha kuwa wakabidhi shule kwa mnunuzi huyo na shamba la Simbani .
"Kama kamati ya siasa ya CCM wilaya walihoji na kuomba kama nunuzi amepewa barua ya kukabidhiwa shule haiwezekani apewe na shamba labla alete barua nyingine "
"Ambapo muda haukupita tukaambiwa kuliletwa barua nyingine kuwa shamba hilo nalo apewe,kwa kuwa Mali za jumuiya kama ni maazi yao sasa sisi ni washauri lakini hatukupewa nafasi ya kushauri" alisema Bundala.
Bundala alisema igewezekana wangeombea hata mkopo lakini viongozi hawa wameamua kuuza ila anaimani viongozi wa CCM taifa watalifuatilia kama kutakuwa na ulazima.
Shule ya sekondari Pwani licha ya kuuzwa lakini eneo hilo halijaanza kushughulikiwa kwa kazi yoyote na badala yake bango la kuonyesha shule ilipo limetolewa na ng,ombe wamegeuza ni sehemu yao ya mapumziko na malisho
0 comments:
Post a Comment