Sunday, April 8, 2018

Published April 08, 2018 by with 0 comment

Waziri Mwakyembe Awaasa Watanzania Kupambana Na Viashiria Vinavyo Sababisha Mauaji Ya Kimbari

Na: Mwandishi wetu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe, amewaasa Watanzania kuhakikisha wanapambana na viashiria vyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na mauaji ya kimbari. Kauli hiyo  Dkt. Mwakyembe ameitoa wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu za mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda miaka 24 iliyopita.

Kwenye hotuba yake Dkt. Mwakyembe amesema mauaji ya kimbari hayatokei ghafla bali huanza kwa chokochoko na kauli za kichochezi ambazo zina lengo la kuigawa jamii vipande vipande. 
“Kilichotokea Rwanda ni fundisho kwetu, mauaji ya kimbari hayatakiwi kutokea tena. Kuhakikisha hayatokei lazima tuyadhibiti mambo yote yanayoweza kuligawa taifa kwa faida ya kizazi cha leo, kesho na keshokutwa” Dkt. Mwakyembe alisisitiza.

Kuendelea kutia mkazo wa ujumbe wake Dkt. Mwakyembe aliinukuu kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, aliyoitoa wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Rwanda  ambapo alisema “haya hayatatokea tena, hatuwezi kubadili kilichotokea awali, lakini tunaweza kubadilisha hali ya leo na hata ya baadae”.

Balozi wa Rwanda nchini mheshimiwa Eugine Kayihura ameishukuru Serikali na wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kuwa pamoja na Wanyarwanda. Pia ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kindugu kati ya Tanzania na Rwanda kwa maendeleo ya watu wake.

Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez amesema nchi zote zina wajibu wa kuwalinda wananchi wake dhidi ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Pia zinatakiwa kuhakikisha zinaungana kupambana na mtu au kikundi chochote chenye nia ya kutekeleza uhalifu kama huo.

Kumbukumbu za mauaji ya kimbari ya Rwanda huadhimishwa kila mwaka na mwaka huu maadhimisho hayo kwa Tanzania yamefanyika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City ambapo Dkt. Mwakyembe alikuwa mgeni rasmi. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwemo mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, watu mashuhuri, viongozi wa serikali na mashirika ya kimataifa na wanafunzi wa shule za sekondari za jijini Dar-es-salaam
Read More
      edit
Published April 08, 2018 by with 0 comment

Picha: Rais Magufuli Akiwa katika Ibada ya Kumsimika Askofu Jimbo la Katoliki la Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameshiriki katika Ibada ya kumsimika Mhashamu Isaack Amani kuwa Askofu Mkuu Jimbo la Katoliki la Arusha katika Kanisa la Mtakatifu Theresia la Mtoto Yesu Jimbo Kuu Katoliki jijini Arusha leo April 8, 2018.
Read More
      edit
Published April 08, 2018 by with 0 comment

BREAKING: Mhariri wa Gazeti la The Guardian aokotwa Bunju akiwa hajitambui

 Mmoja wa wahariri waandamizi wa gazeti la The Guardian, Finnigan Simbeye ameokotwa eneo la Bunju wilayani Kinondoni akiwa hajitambui.

Taarifa zilizosambaa leo Jumapili Aprili 8, 2018  zinazoonyesha kitambulisho chake cha kazi cha kampuni ya The Guardian Limited zinaeleza Simbeye aliokotwa akiwa kwenye hali mbaya.

Hata hivyo, kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni, Murilo Jumanne amesema hana taarifa za tukio la kuokotwa Simbeye.

Rose Mirondo, ambaye ni mkewe Simbeye amesema mumewe aliondoka nyumbani jana Jumamosi Aprili 7, 2018 akiwa na gari lakini hakurudi hadi alipopata taarifa za kuokotwa kwake leo.

Amesema alipokwenda eneo la tukio Bunju hakuliona gari la mumewe.

Rose amesema watu aliowakuta eneo la tukio wamemweleza kwamba Simbeye alichukuliwa na polisi kupelekwa hospitali.

Amesema bado hana taarifa ya hospitali gani amepelekwa na kwamba, anakwenda Kituo cha Polisi Bunju kupata taarifa zaidi.
Read More
      edit
Published April 08, 2018 by with 0 comment

Meya aliyesifiwa na Rais afunguka kuhusu kuhama


Meya, Wajiji la Arusha, Kalista Lazaro (CHADEMA) amefunguka na kusema kitendo cha Rais kumsifia mbele ya hadhara ni heshima kwake na viongozi wa Arusha na kusema hakuna sababu kiongozi aliyechaguliwa na wananchi kuhama chama kwa kumuunga mkono Rais.

Kalista Lazaro alisema hayo April 7, 2018 baada ya Rais Magufuli kumsifia kuwa ni kati ya watu ambao wanapenda maendeleo na kufanya maendeleo katika jiji la Arusha Mjini licha ya kiongozi huyo kutokea katika chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

"Hii pongezi ya Rais ni kwa sababu alipokea taarifa ya utendaji ya jiji la Arusha na tangu alipoingia nilimweleza mambo ambayo tumefanya kwa mfano amepongeza jitihada kubwa ya ujenzi wa madarasa tangu mwaka 2016 ambapo tumejenga madarasa 105, 2017 tumejenga madarasa 61
"Tunapandisha vituo vya afya mara moja na dispensary kwa ujumla tano, hospitali ya wilaya, barabara za lami, barabara za vumbi na juzi tumetangaza tenda ya kilometa 10 za lami katika jiji la Arusha ambapo barabara ya Njiro, Kwa Mlombo, Sombetini zinaenda kujengwa lami pamoja na barabara ya Ngarenalo kwangu mimi ni heshima na hii heshima nimeipokea kwa niamba ya wananchi wa jiji la Arusha" alisema Kalista Lazaro

Aidha Kalista Lazaro amedai kupongezwa kwake kuwe funzo kwa viongozi wengine ambao wamekuwa wakihama kutoka CHADEMA na kwenda CCM kwa kigezo cha kuunga mkono serikali na kudai kuwa ukitaka kufanya hivyo unachotakiwa kutekeleza tu yale uliyoahidi kwa wananchi wako na si kwa kigezo cha kuhama chama.

"Wale ambao walikuwa wanabeza na hawatambui sasa wametambua kuwa Meya wao anapongezwa na Rais Magufuli mbele ya halaiki ya watu, mbele ya polisi, mbele ya Mkuu wa Majeshi hivyo Rais anaona kazi tunayofanya na niwaambie wananchi hakuna sababu ya kiongozi wa kuchaguliwa kuhama, ukitaka kutekeleza wajibu wako na kuunga mkono serikali unatakiwa ufanye kazi ambayo umeahidi wananchi wako. Mimi leo napongezwa nikiwa ndani ya CHADEMA, nikiwa Meya wa CHADEMA na diwani wa CHADEMA kwangu mimi ni heshima" alisisitiza
Read More
      edit
Published April 08, 2018 by with 0 comment

Serikali Kuanzisha Kampeni Ya Jiongeze Tuwavushe Salama ili kupunguza vifo vya Mama na Mtoto

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amesema matatizo ambayo yanatokana na uzazi yapo ambayo yanaweza kuzuilika na kuhimiza wadau kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuendelea kupunguza vifo vya mama mjazito na mtoto.

Pia ametoa pongezi kwa hatua zinazochukuliwa na Taasisi ya Childbirth Survival International(CSI) ya kuhakikisha wanatoa elimu ya afya salama ya uzazi na kushiriki kwa vitendo katika kufanikisha vifo kwa mama na mtoto vinapungua hapa nchini.

Amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akitoa hotuba yake kwenye Maadhimisho ya miaka mitano ya CSI na kutumia nafasi hiyo kuwapongeza waanzilishi wa taasisi hiyo Stella Mpanda na Profesa Tausi Kagasheki.

Rais mstaafu Kikwete amesema kumekuwepo na vifo ambavyo vinatokea kwa wajawazito na watoto ambao hawana hatia na kutumia nafasi hiyo kuhimiza wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kupunguza vifo hivyo.

Amesema ipo haja ya kuendelea kutolewa elimu ambayo itasaidia jamii kutambua umuhimu wa kuhudhuria kliniki kwa mama mjazito na kubwa zaidi kuendelea kutatua changamoto zilizopo kwenye eneo la afya ya uzazi na vifo. Ameelezea hatua ambazo zinachukuliwa katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

“Nimefurahi sana kuona taasisi hii imenzishwa na akina mama wa Tanzania. Stella Mpanda yeye ni mkunga na Tausi yeye ni mwanataaluma .Nifaraja sana wamama wa Tanzania kufanya jambo kubwa kama hili la kuhakikisha wanashiriki katika kupunguza vifo vya wajawazito,

“Wametoa heshima kubwa kwa nchi yetu na pia wamefanya jambo kubwa kwa wanawake nchini kwa kuanzisha taasisi kubwa kama hii ya CSI. Kwa bahati mbaya akina mama wakati mwingine mnashindwa kupongezana. Adui wa mwanamke ni mwanamke ni mwenyewe,” amesema Rais mstaafu Kikwete.

Kuhusu changamoto zilizopo kwenye afya ya uzazi na kwamba moja ya malengo ya milenia inazungumzia kupunguza vifo vya mama mjazito na watoto chini ya miaka mitano.

“Wakati naingia madarakani mwaka 2005 , vifo kwa watoto wanaokufa ilikuwa 578 kati ya vizazi hai 100,000 wanaozaliwa. Baadae tukapunguza vifo hadi watoto 432 lakini ikapanda tena hadi vifo vya watoto 556 wakati lengo la milenia ilikuwa ni watoto 191,

“Hivyo tukaamua kuweka mikaka katika kuhakikisha tunapunguza vifo hivyo,” amesema.

Hata hivyo takwimu za mwaka 2016 kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni kwamba kati ya vizazi hai 100,000 wanaopoteza maisha ni 556.

Serikali kuja na Kampeni ya JIONGEZE TUWAVUSHE SALAMA
Kwa upande wa Waziri  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema wanatarajia kuanzisha kampeni   itakayofahamika Jiongeze tuwavushe salama.

Amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha mama mjazimto anajiongeza kwa kuhakikisha anakwenda kituo cha afya na akifika anayetoa huduma naye ajiongeze kwa kutoa huduma sahihi ambayo mtamuwezesha mjazmito kujifungua salama.

Waziri Mwalimu ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua ambazo Serikali ya awamu ya tano inavyochukua jukumu la kuhakikisha vifo vya mama mjazito na mtoto vinapungua ambako akagusia kampeni hiyo.

“Tumeongeza bajeti ya wizara ya afya na sehemu kubwa pamoja na kuangalia dawa na vifaa tiba pamoja na miundombinu pia tumeweka nguvu katika afya ya mama na mtoto,” amesema.

Wakati huo huo Mwalinzishi na Mkurugenzi wa CSI Stella Mpanda ameelezea namna ambavyo taasisi yao imejikita katika kuhakikisha vifo vya mama mjazito na mtoto vinaungua na kufafanua kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya uzazi.
Read More
      edit

Saturday, April 7, 2018

Published April 07, 2018 by with 0 comment

TUCTA Nao Wataka Watumishi Darasa la 7 Warudishwe Kazini

Baraza Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) jana Jumamosi Aprili 7, 2018 limetoa tamko lenye mambo saba, likiwemo la kupinga uamuzi wa Serikali kuwafuta kazi watumishi wake wenye elimu ya darasa la saba.

Akisoma tamko hilo mbele ya wajumbe wa baraza kuu la Tucta katika mkutano wa baraza hilo uliofanyika mkoani Morogoro mwenyekiti wa Tucta, Tumaini Nyamhokya alisema uamuzi huo wa Serikali si sahihi na hivyo wametaka watumishi hao kurejeshwa kazini.

Alisema baraza limesikitishwa na uamuzi wa kuwaondoa kazini watumishi wa umma na taasisi zinazopokea ruzuku kutoka serikalini.

Nyamhokya alisema uamuzi huo si wa kisheria ikizingatiwa kuwa watumishi hao waliajiriwa kwa kufuata taratibu halali za ajira.

“Kwa hiyo Tucta tunaitaka serikali kutengua uamuzi wake na kuwarudisha watumishi hao kazini bila kupoteza haki zao za kiutumishi kwa kipindi chote,” alisema.

Mambo mengine sita yaliyopo katika tamko hilo wanayotaka yafanyiwe kazi ni; ongezeko la mishahara, kodi ya mishahara (PAYE), kupandishwa madaraja na vyeo kwa watumishi wa umma, malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi na watumishi kwa baadhi ya taasisi, ucheleweshwaji wa malipo ya wastaafu kwa baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii na uamuzi wa Serikali kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.
Read More
      edit
Published April 07, 2018 by with 0 comment

Viongozi wa kitaifa,Wazungumzia maendeleo yaliyoachwa na Rais wa kwanza Z'bar

Viongozi wa Kitaifa kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wamesema Watanzania wanaendelea kumkumbuka Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kutokana na Maendeleo makubwa aliyoyafanya wakati wa Uongozi wake miaka minane na kufanikiwa kuacha historia isiyofutika kwa kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar na tukio la kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania April 26, mwaka 1964.

Viongozi hao wametoa kauli jhiyo jana kwa nyakati tofauti, muda mfupi baada ya kukamilika kwa shughuli ya kumbukumbu ya miaka 46 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume iliyofanyika katika ofisi kuu ya Chama cha Mapinduzi iliyopo Kisiwandui visiwani hapa.

Walisema yanayooneka hivi sasa Zanzibar yametokana na dira ya maendeleo iliyoachwa na Marehemu Abeid Amani Karume ya kuwaletea wananchi Maendeleo katika sekta mbalimbali kwa kuondosha matabaka na kufanikiwa kujenga umoja wa kitaifa pamoja na kuasisi Muungano ambao umevunja rekodi kwa kudumu zaidi ya miaka 50.

Kila ifikapo April 7 kila mwaka, Watanzania huadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ambaye aliuwawa na Wapinga Maendeleo na kuacha simanzi na majonzi kwa wanaharakati wa ukombozi wa Bara la Afrika.
Read More
      edit
Published April 07, 2018 by with 0 comment

Profesa Jay akumbuka msoto wa Maisha....Asimulia Alivyokuwa Anakunywa Maji ya Chooni na Kupanda Malori

Nguli wa muziki wa Bongo Fleva ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mikumi, Joseph ‘Profesa Jay’ Haule, amekumbuka msoto aliokutana nao wakati anatafuta kutoka kimuziki miaka ya 1990 akiwa na Hard Blasters Crew (HBC).

Akifunguka kupitia The Playlist ya Times FM, rapa huyo mkongwe aliyechonga barabara kwa wasanii wengi wa rap nchini, amesema kuwa wakati wanaandaa albam zao na HBC, hawakuwa na kitu mfukoni kiasi cha kufikia hatua ya kunywa maji ya bomba lililokuwa chooni ili waendelee kufanya kazi yao studio.

“Nakumbuka wakati huo tunarekodi, unaenda kunywa maji chooni hivi… kwenye bomba liliko chooni unakula na mihogo yako ili uweze ku -buy time ya kuendelea kuwa studio siku nzima. Kwamba hakuna hata pesa ya kula chips mzee,” Profesa alifunguka.

Mkali huyo wa rap mwenye majina mengi ya kupewa kwa kuwa mbabe wa kurap, alieleza kuwa wakati wamepata nafasi ya kurekodi albam yao kama HBC, kuna wakati akiwa anafanya kazi Tanga, ilimlazimu kupanda malori ya mizigo usiku ili arejee kazini Jumapili usiku, kwani muda wa usiku aliokuwa akimaliza kurekodi jijini Dar es Salaam, magari ya abiria hayakuwepo.

Katika hatua nyingine, Profesa Jay alieleza tukio la kurekodi wimbo wake wa ‘Jina Langu’ katika studio za Bongo Records chini ya mtayarishaji nguli, P-Funk Majani. Alisema alimshangaza Majani kwani alikuwa akisikia mara kadhaa mdundo wa wimbo huo, ndipo alipomuomba mtayarishaji huyo aingize sauti.

Alisema baada ya kuwekewa mdundo, alipita na mashairi yote matatu bila kukwama, kitu ambacho kilimshangaza Majani pamoja na ukubwa wa mashairi yaliyowekwa ndani.

Profesa amewashauri wasanii wa Tanzania kuendelea kuandika vitu ambavyo vinagusa jamii na kuitangaza Tanzania kwa maslahi ya taifa kwa ujumla.

Hivi karibuni, aliachia wimbo wake ‘Pagamisa’ akiwa na mtayarishaji wa muziki, Mr. T-Touch.
Read More
      edit
Published April 07, 2018 by with 0 comment

Polisi 458 Wafukuzwa Kazi

Jumla ya maofisa wa Jeshi la Polisi wapatao 458 wamefukuzwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu kuanzia mwaka 2015 hadi Machi mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa jana Aprili 7 na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro alipokuwa akizungumza mbele ya Rais John Magufuli wakati wa uzinduzi wa nyumba 31 za Polisi na ufunguzi wa kituo cha Polisi cha Utalii na Kidiplomasia jijini Arusha.

Sirro alisema kazi ya Jeshi la Polisi ni kurekebisha mienendo ya wananchi, hivyo kabla hawajawaelimisha wananchi wanapaswa kuwa na mienendo mizuri wao kwanza.

Alifafanua kwa kulitambua hilo ndiyo maana askari waliokwenda kinyume na azma hiyo walichukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi, ambapo kwa mwaka 2015, 198 walifukuzwa kazi.

Alisema kwa mwaka 2016 walifukuzwa askari 165, 2017 (81) na kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu wamefukuzwa askari 14.

“Hatuna muhali kuwachukulia hatua askari wanaokiuka utaratibu na nidhamu ya utendaji katika Jeshi la Polisi,” alisema IGP Sirro.
Read More
      edit
Published April 07, 2018 by with 0 comment

Baba Mzazi: 'Abdul Nondo babu yake ni muasisi wa TANU'

Abdul Nondo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye anakabiliwa na kesi ya kujiteka mwenyewe, mzazi wake Omar amethibitisha kuwa baba yake alizaliwa mwaka 1919 huko Ujiji, Kigoma na kuwa ni miongoni mwa waasisi wa chama cha Tanu.

Mzee Omar, alisema baba yake huyo aliyemtaja kwa jina la Omar Kagobe alipata watoto 30, mmoja akiwa yeye.

“Nashangaa hao wanaomkamata na kumhoji mtoto wangu kuwa sio raia, wananichekesha sana kwa kuwa najua mwisho wa siku watajua ukweli wake. Ukweli ni kwamba wazazi wangu ndio waasisi wa Tanu na walishiriki kikamilifu katika kupigania uhuru wa nchi hii, hivyo suala hilo halinipi wasiwasi wala hofu na hivyo vyeti wanavyovitaka mbona vipo tu, ila waelewe kuwa sisi ni Wamanyema halisi na ni raia halali wa nchi hii,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa ACT - Wazalendo, Mkoa wa Kigoma, Sendwe Mbaruku, alitoa taarifa Alhamisi kuhusu suala la Nondo kuhojiwa na uhamiaji na kusema; “Kijana Abdul ni mtoto wetu hapa Kigoma, wazazi wake ni wakazi na wapiga kura wa hapa Ujiji, zaidi ni Watanzania wenzetu.”

Maelezo haya yametolewa na mzazi huyo Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu uraia wake.

Mzazi huyo amesema babu yake Nondo, alishawahi kuwa Polisi kwa miaka 18 kuanzia mwaka 1940 hadi 1958 na alishafanya kazi huko Mabatini mkoani Mwanza na sehemu nyingine za nchi.

Alisema babu yake wakati akiwa polisi, ndipo zilipoanzishwa Kota za Msimbazi, Dar es Salaam na jina lake lilikuwa maarufu, akijulikana kama Mzee Kagobe.

Kama haitoshi alisema bibi yake Nondo alikwenda kuhiji, mnamo 1970 na alipewa hati ya kusafiria ya Tanzania, huku akihoji, “Kama angekuwa sio raia wa Tanzania angepewaje hati hiyo?”

Baada ya Nondo kuripoti polisi mjini Mafinga alishikiliwa na jeshi hilo Mkoa wa Iringa na baadaye kukabidhiwa kwa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema kupitia uchunguzi wa kisayansi, wamebaini kuwa hakuwa ametekwa, bali alijiteka na tayari suala lake lipo mahakamani, Iringa.
Read More
      edit
Published April 07, 2018 by with 0 comment

Mbunge Mchafu aitaka Serikali kupitia Sheria upya

Wakati Wabunge walikuwa wakichangia mapendekezo yao katika  bajeti ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2018/19   Mbunge wa viti maalum CCM Hawa Mchafu Chakoma  ameishauri serikali kuanzisha namna bora ya  mpango wa pensheni kwa wazee waliolitumikia taifa.

Hawa Mchafu alisema ;"Nashindwa kufahamu mfuko wa moja kwa moja ambao upo kwa ajili ya wazee, muda umefika sasa ule mchakato wa pensheni kwa wazee uje sasa ili kuweza kuwasaidia wazee wa taifa letu ambao kwa nafasi zao walisaidia sana nchi yetu”

“Niipongeze Serikali pia kwa kuanzisha miradi mbalimbali mikubwa ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta, ujenzi wa viwanja vya ndege n.k  ....ni wazi itaambatana na upatikanaji wa ajira lakini niishauri Serikali ihakikishe inafuatilia mikataba ya kazi kwa watanzania inayofanyika katika miradi hiyo kwamaana kumekuwa na ukakasi mkubwa sana mikataba mingi inaukiukwaji wa kisheria” –Hawa Mchafu
Read More
      edit
Published April 07, 2018 by with 0 comment

Mwanamke wa Kwanza Kupata Degree Tanzania Atunukiwa Tuzo

Dkt Maria Kamm ndiye  mwanamke wa kwanza wa Tanzania kupata Shahada ya kwanza (Degree) na jana ametunukiwa tuzo ya heshima katika tuzo za Malkia wa Nguvu zinazoandaliwa na Clouds Media.

Mama Kamm ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Weruweru iliyopo Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, akiwa kama Mzalendo wa kweli, ametumia maisha yake kwa kiasi kikubwa kuwashauri na kuwaelimisha vijana katika masuala mbalimbali ya Taifa.

Mgeni Rasmi katika utoaji wa Tuzo hizo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwl Nyerere Posta jijini Dar, alikuwa Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dr. Ummy Ally Mwalimu.
Read More
      edit
Published April 07, 2018 by with 0 comment

Serikali Yapata Mkopo Wa Shilingi Bilioni 34 Kutoka Mfuko Wa Maendeleo Ya Kiuchumi Wa Kuwait

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kiuchumi wa Kuwait (Kuwait for Arab Economic Development Fund), na Serikali ya Tanzania zimetiliana saini  rasimu ya mkataba wa  kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola milioni 15.3, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 34, kwa ajili ya mradi wa  kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Luiche, mkoani Kigoma,  lenye ukubwa wa  hekta 3,000.

Rasimu hiyo ya Mkataba imesainiwa na Kiongozi wa ujumbe wa wataalamu na Mshauri wa Masuala ya Kilimo wa Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait,  Dkt. Abdulrida Bahman na  kwa upande wa Tanzania ikisainiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, mjini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)  amesema hatua hiyo imfikiwa baada ya timu ya wataalamu kutoka Kuwait kutembelea eneo la mradi mkoani Kigoma na kuridhishwa na umuhimu wake kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

 “Mradi huo una umuhimu mkubwa kwa watanzania kwa kuwa wataweza kuwa na kilimo cha umwagiliaji cha Mpunga na Mbogamboga kwa mwaka mzima badala ya kilimo cha msimu cha kutegemea mvua, na katika siku zijazo Kigoma itakua miongoni mwa mikoa inayozalisha mchele kwa wingi”, alisema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali ya Tanzania na Kuwait zitatia saini mkataba rasmi wa mkopo huo wenye masharti nafuu ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu ili mradi huo uanze kutekelezwa ili kuongeza kipato cha wananchi na  kuwa na uhakika wa chakula.

Amesema Nchi ya Kuwait imekuwa ikiisaidia Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ukarabati wa Hospitali ya Mnazi mmoja, Zanzibar kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 13.6 sawa na shilingi bilioni 31.

"Kwa upande wa Tanzania Bara wametoa mkopo nafuu wa shiingi bilioni 115 kwa ajili ya kuboresha barabara ya Chaya hadi Nyahua (km 85) kwa kiwango cha lami ambayo ni muhimu kwa kuwa inaunganisha mikoa ya Magharibi mwa Tanzania" aliongeza Dkt. Mpango

Miradi mingine ambayo  nchi hiyo imeonesha nia ya kuisaidia nchi, ni pamoja na ujenzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza, uboreshaji wa barabara ya kutoka Morogoro hadi Dodoma na ujenzi wa barabara za mzunguko za kuingia na kutoka mjini Dodoma ambazo zitasaidia kuondoa msongamano wa magari yanayopita katikati ya mji huo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na vyombo vya moto baada ya Makao Makuu ya Serikali kuhamia Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mpango ameishukuru nchi ya Kuwait kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait, kwa nia yake njema na thabiti katika kusaidia nchi ya Tanzania kutekeleza kwa mafanikio miradi ya Maendeleo ya kiuchumi katika nia yake ya kupata maendeleo Stahiki.

Kwa upande wake Kiongozi wa ujumbe wa wataalamu na Mshauri wa Masuala ya Kilimo wa Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait, Dkt. Abdulrida Bahman, ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Fedha na Mipango kwa ukarimu pamoja na Idara ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ushirikiano mzuri katika hatua za kufanikisha utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji  wa Bonde la Luiche, Mkoani Kigoma.

“Tumetembelea eneo la mradi kwa takribani wiki mbili tumejionea uzuri wa nchi hii na fursa zilizopo, hii ni nchi tajiri na inaweza kuwa tajiri kuliko Kuwait kwa kuwa kila kitu kinachoweza kufanya nchi hii iwe tajiri kipo”.Alieleza Dkt. Bahman.

Amesema mradi huo wa umwagiliaji hautakuwa wa mwisho kupewa fedha na mfuko huo bali utaendelea kusaidia kutekeleza miradi mingine mingi kama ilivyokuwa ikifanya, kutokana na ushirikiano mzuri, wa kihistoria, na wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Mwisho.
Read More
      edit